Waraka wa Kwanza wa Jenerali wa Yohana
SURA YA 1
Yohana anashuhudia injili.
1 Ndugu zangu, huu ndio ushuhuda tunaoutoa wa yale yaliyokuwako tangu mwanzo, tuliyosikia, tuliyoyaona kwa macho yetu, tuliyoyatazama, na mikono yetu kulishika, wa Neno la uzima;
2 (Kwa maana uzima ule ulidhihirishwa, nasi tumeuona, na twashuhudia, na kuwaonyesha ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirishwa kwetu;)
3 Hilo tuliloliona na kulisikia twawahubiri ninyi, ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi; na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwanawe Yesu Kristo.
4 Tunawaandikia ninyi mambo haya ili furaha yenu ikamilike.
5 Basi, hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala hamna giza hata kidogo ndani yake.
6 Tukisema kwamba tuna ushirika naye, lakini tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli.
7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
8 Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani yetu.
9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu.
SURA YA 2
Kristo mtetezi wetu - Maovu ya ulimwengu yaepukwe - Upako wa Roho.
1 Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Lakini kama mtu akitenda dhambi na kutubu, tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki;
2 Naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.
3 Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake.
4 Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.
5 Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli; katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake.
6 Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.
7 Ndugu, ninawaandikia ninyi amri mpya, lakini ndiyo ileile mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri ya zamani ni neno mlilolisikia tangu mwanzo.
8 Tena, amri mpya ninayowaandikia, ambayo iliamriwa zamani na Mungu; na ni kweli ndani yake, na ndani yenu; kwa sababu giza linapita ndani yenu, na nuru ya kweli sasa inang'aa.
9 Yeye asemaye yumo nuruni, naye anamchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.
10 Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.
11 Lakini anayemchukia ndugu yake yu gizani na anatembea gizani, wala hajui aendako, kwa sababu giza limempofusha macho.
12 Ninawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu kwa ajili ya jina lake.
13 Nawaandikia ninyi akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Ninawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmemjua Baba.
14 Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.
15 Msiipende dunia, wala mambo ya dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
16 Kwa maana kila kilichomo duniani ambacho ni cha tamaa ya mwili, na tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake; bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.
18 Watoto wadogo, ndiyo wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga-Kristo atakuja, hata sasa kuna wapinga Kristo wengi; kwa hiyo twajua ya kuwa ni mara ya mwisho.
19 Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu; kwa maana kama wangalikuwa wa kwetu, bila shaka wangalikaa pamoja nasi; lakini walitoka ili wadhihirishwe kwamba wote hawakuwa wa kwetu.
20 Lakini ninyi mmepakwa na Yeye Aliye Mtakatifu, nanyi mnajua mambo yote.
21 Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamuijui iliyo kweli, bali kwa sababu mnaijua, na kwamba hakuna uongo utokao katika kweli.
22 Ni nani aliye mwongo isipokuwa yeye anayekana kwamba Yesu ni Kristo? Yeye ni mpinga-Kristo, anayemkana Baba na Mwana.
23 Kila amkanaye Mwana, huyo hana Baba; bali yeye amkiriye Mwana anaye Baba pia.
24 Basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hayo mliyoyasikia tangu mwanzo yakikaa ndani yenu, mtakaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba pia.
25 Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.
26 Nimewaandikia ninyi mambo haya kuhusu wale wanaowapotosha.
27 Lakini upako mlioupokea kwake unakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama upako huo unavyowafundisha mambo yote, tena ni kweli, wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.
28 Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake; ili, atakapotokea, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake katika kuja kwake.
29 Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwadilifu, mwajua ya kuwa kila mtu atendaye haki amezaliwa na yeye.
SURA YA 3
Upendo wa Mungu kwa watakatifu - Kuzaliwa upya - Upendo wa Kristo.
1 Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; kwa hiyo ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.
2 Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa, atakapotokea, tutafanana naye; maana tutamwona jinsi alivyo.
3 Na kila mtu aliye na tumaini hili ndani yake anajitakasa kama yeye alivyo mtakatifu.
4 Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa maana dhambi ni uvunjaji wa sheria.
5 Nanyi mnajua kwamba yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi zetu; na ndani yake hamna dhambi.
6 Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila adumuye katika dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.
7 Watoto wadogo, mtu awaye yote asiwadanganye; atendaye haki ni mwenye haki, kama yeye alivyo mwadilifu.
8 Anayedumu katika dhambi ni wa Ibilisi; kwa maana Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.
9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hadumu katika dhambi; kwa maana Roho wa Mungu hukaa ndani yake; wala hawezi kudumu katika dhambi, kwa sababu amezaliwa na Mungu, akiisha kupokea Roho Mtakatifu wa ahadi.
10 Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi; mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.
11 Kwa maana hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi.
12 si kama Kaini, aliyekuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Na kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake mwenyewe yalikuwa maovu, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.
13 Ndugu zangu, msistaajabie ulimwengu ukiwachukia.
14 Tunajua kwamba tumepita kutoka kifo hadi uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Yeye asiyempenda ndugu yake, yuko katika kifo.
15 Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji; nanyi mnajua kwamba kila muuaji hana uzima wa milele ndani yake.
16 Katika hili tumelifahamu pendo la Kristo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; na imetupasa sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.
17 Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia hii kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji na kumzuilia huruma yake, je, upendo wa Mungu wakaaje ndani yake?
18 Watoto wangu wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi tu; bali kwa vitendo na kweli.
19 Na katika hili twajua ya kuwa sisi ni wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake.
20 Kwa maana ikiwa mioyo yetu inatuhukumu, Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu, naye anajua yote.
21 Wapenzi, ikiwa mioyo yetu haituhukumu, basi tuna ujasiri kwa Mungu.
22 Na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kufanya yale yampendezayo machoni pake.
23 Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotuamuru.
24 Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake, naye ndani yake. Na katika hili twajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.
SURA YA 4
Jaribu roho - Ubora wa upendo - Mungu ni upendo.
1 Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea duniani.
2 Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; Kila roho inayokiri kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu;
3 Na kila roho isiyokiri kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili haitokani na Mungu; na hii ndiyo roho ya mpinga-Kristo, ambayo mmesikia kwamba inakuja; na hata sasa tayari iko ulimwenguni.
4 Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu na mmewashinda; kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.
5 Wao ni wa ulimwengu; kwa hiyo wanena ya dunia, na ulimwengu huwasikia.
6 Sisi ni wa Mungu; yeye amjuaye Mungu hutusikia; asiye wa Mungu hatusikii. Katika hili twamjua roho wa kweli na roho wa upotevu.
7 Wapenzi, na tupendane; kwa maana pendo latoka kwa Mungu; na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu.
8 Yeye asiyependa, hamjui Mungu; kwa maana Mungu ni upendo.
9 Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu alimtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye.
10 Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.
11 Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana sisi kwa sisi.
12 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote, isipokuwa wale wanaoamini. Tukipendana, Mungu anakaa ndani yetu, na upendo wake unakamilishwa ndani yetu.
13 Katika hili twajua ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametupa Roho wake.
14 Na sisi tumeona na kushuhudia kwamba Baba alimtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu.
15 Kila anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu.
16 Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo; naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu ndani yake.
17 Upendo unakamilishwa ndani yetu ili tuwe na ujasiri siku ya hukumu. kwa sababu kama yeye, ndivyo tulivyo katika ulimwengu huu.
18 Hakuna woga katika upendo; lakini upendo kamili huitupa nje hofu; kwa sababu hofu ina adhabu. Mwenye hofu hakukamilishwa katika upendo.
19 Sisi twampenda kwa sababu yeye alitupenda sisi kwanza.
20 Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezije kumpenda Mungu ambaye hakumwona?
21 Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu ampende na ndugu yake.
SURA YA 5
Kuzaliwa upya—Mashahidi wanaotoa ushuhuda wa uzima wa milele.
1 Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu; na kila ampendaye mzaa ampenda pia yeye aliyezaliwa na yeye.
2 Katika hili twajua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, tunapompenda Mungu, na kuzishika amri zake.
3 Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; na amri zake si nzito.
4 Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.
5 Ni nani anayeushinda ulimwengu isipokuwa ni yeye aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?
6 Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si kwa maji tu, bali kwa maji na damu. Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli.
7 Kwani wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu; na watatu hawa ni umoja.
8 Na wako watatu washuhudiao duniani, Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana katika hali moja.
9 Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushahidi wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana huu ndio ushuhuda wa Mungu ambao amemshuhudia Mwana wake.
10 Amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake; asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo; kwa sababu hakuuamini ushuhuda ambao Mungu alitoa juu ya Mwanawe.
11 Na huu ndio ushuhuda, kwamba Mungu alitupa uzima wa milele, na uzima huu umo katika Mwana wake.
12 Aliye naye Mwana anao huo uzima; na asiye na Mwana wa Mungu hana huo uzima.
13 Nimewaandikia ninyi mambo haya ninyi mnaoliamini jina la Mwana wa Mungu; ili mjue kwamba mna uzima wa milele, na kuendelea kuliamini jina la Mwana wa Mungu.
14 Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia;
15 Na ikiwa tunajua kwamba anatusikia, chochote tunachoomba, tunajua kwamba tunayo maombi tuliyomwomba.
16 Mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, naye atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Kuna dhambi ya mauti; Sisemi kwamba ataiombea.
17 Udhalimu wote ni dhambi; na kuna dhambi isiyo ya mauti.
18 Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hakai katika dhambi; lakini yeye aliyezaliwa na Mungu na kujilinda, yule mwovu hawezi kumshinda.
19 Tunajua kwamba sisi ni wa Mungu, na kwamba ulimwengu wote unakaa katika yule mwovu.
20 Na tunajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja, na ametupa sisi akili ili tumjue yeye aliye wa kweli; nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.
21 Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu. Amina.
Maktaba ya Maandiko: Toleo la Biblia Lililopuliziwa
Kidokezo cha Utafutaji
Andika neno moja au tumia manukuu kutafuta kifungu kizima (km "kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu").
Kwa rasilimali za ziada, tafadhali tembelea yetu Rasilimali za Wanachama ukurasa.